Friday, 25 May 2012

KUJITOA NA KUTOA KWA AJILI YA BWANA

Tunaposoma kitabu cha 1 cha Mambo ya Nyakati 29:5c tunaona Mfalme Daudi anauliza swali, "Ni nani basi ajitoaye kwa moyo ili ajiweke wakfu leo kwa BWANA?
Nataka tuangalie jinsi ya kujitoa na kutoa kwa ajili ya BWANA. Tunapoandaa Mkutano wa Injili tunatazama kwa agizo la BWANA YESU la kutoka na kupeleka Neno la MUNGU kwa watu wote. Mathayo 28:19. Kwa maana kila mwanadamu aliyeumbwa kwa mfano wa MUNGU na sura ya MUNGU anatakiwa kufikiwa na Nuru ya Injili. Awe yule aliye Mkristo kwa maana ya kubatizwa na yule asiye Mkristo, wote wanatakiwa kufikiwa na neema ya Neno.

Pili, kusudi la Mkutano wa Injili ni kuwaleta watu wote kwa BWANA YESU KRISTO ili wamkiri YESU kuwa ni BWANA na Mwokozi wa maisha yao. Warumi 10:13 Kila atakayeliita jina la BWANA ataokoka.

NAMNA YA JINSI YA KUWAFIKIA

Mfalme Daudi anasema na watu wa taifa lake anataka kujua, anataka kuwatambua wale walio tayari kwa kujitoa kwao kwanza kwa BWANA kwa moyo wa dhati. Anaujua mwanadamu anasema na moyo kwanza kabla ya kujitoa kwake BWANA.

Moyo: Moyo wa mwanadamu ni kama kiunganishi kati ya mwili na roho. Unaposoma kitabu cha Yeremia 17:9-10 utaona jinsi moyo wa mwanadamu ulivyo. Kwa kuwa BWANA anaujua moyo wa mwanadamu, YEYE anachunguza moyo sio roho wala mwili.

Ikiwa sisi leo tutajitoa mioyo yetu kwa BWANA, ndipo kusudi la MUNGU la kuwafikishia watu wengine Nuru ya Injili litafanikiwa. Sio wote tutakuwa wahubiri, bali sisi tunaweza kuhubiri au kuwafikishia wengine neema hiyo kwa kuwapeleka kwa njia ya kuota fedha ili wahubiri waende wakahubiri. Warumi 10:14-15.

MUNGU aseme nasi kwa lugha yake ya upole na upendo mkuu, na tujiweke wakfu kwa BWANA leo.

BARIKIWA.

Wednesday, 23 May 2012

KUMSHUKURU MUNGU KWA KUTOA MAVUNO

Katika maisha ya mwanadamu kuna vitu viwili huwa anapewa au kuvipata kwa njia ya kutunukiwa na kuzawadiwa, navyo ni tuzo na zawadi.

Tuzo kwa kawaida mtu hupewa baada ya kushinda jambo fulani katika shindano mfano katika michezo, nk. Thamani ya tuzo mara nyingi anayejua ni yule aliyekabidhiwa hata namna ya kutunza.

Zawadi ni kitu ambacho mtu anaweza kupewa pasipo kutarajia kupewa au kupata. Mara zote zawadi inaambatana na shukrani kwa aliyetoa kukupatia. Inakulazimu kuiheshimu na kuitunza kwa kwa kuithamini zawadi inawezekana ikiwa ni kitu fulani, mfano; shati, nk.

Mtoaji siku zote angefurahia nakufikiria zaidi kama atakukuta nacho. Inawezekana angefikiria kukupa kikubwa zaidi. Lakini akifika kwako na kukuona unachezea ile zawadi aliyokupa nafikiri atachukia au kuwa na mawazo mengi kichwani.

Na ndivyo ilivyo kwetu sisi wanadamu. MUNGU wetu ametupa zawadi nyingi za thamani lakini si mara zote tmeweza kuzienzi hizo zawadi au hata kuzitumia vema.

Kumbukumbu la Torati 8:12-14. 17-18 mwandishi anasema, Angalia mwanadamu, neema ya MUNGU utakapobarikiwa na BWANA na mafanikio ya kimaisha utakapofanikiwa kumbuka kumshukuru MUNGU wako maana ndiye aliyekufanikisha.

Daudi aliliona hilo kweli kuwa ni nguvu za MUNGU katika Zaburi akajiuliza swali, mimi nitamrudishia nini BWANA kwa ukarimu wote? Zaburi 11:12.

Ewe mwanadamu, fikiri kwa mapana na kwa kina sana kwa jinsi MUNGU wako alivyokufanikisha.

BARIKIWA.

Wednesday, 2 May 2012

SADAKA YA SHUKRANI

Sadaka ya shukrani ni mojawapo ya sadaka zilizo za muhimu sana mbele za MUNGU kwa sababu ni sadaka inayoonyesha na kutambulisha maisha mazima ya mwanadamu.

Sadaka hii ya shukrani inabeba hali ya maisha ya mtu mbele za MUNGU. Mwanadamu lazima ajitambue kuwa yeye si kitu.

KWANINI TUNATOA SADAKA HII

Tunatoa sadaka ya shukrani kuonyesha moyo wa kutaka kumwambia MUNGU asante kwa yote aliyotutendea na anayoendela kututendea.

Ukisoma Zaburi 111:1-6, Mfalme Daudi kwa kutambua nguvu, uwezo na mamlaka ya MUNGU kwa jinsi ambavyo amempigania, amemtunza, amemlisha, amemshindia majaribu, anafika mahali anasema atamshukuru BWANA kwa moyo wangu wote. Matendo ya BWANA kwake ni mengi mno.

BWANA MUNGU ametufadhili kwa mengi sana, Zaburi 118:1. Tambua kuwapo hai hadi sasa ni mapenzi yake tu. Wewe huna cha kujivunia uzima wako, ni neema ya BWANA mwambie asante.

Mwanadamu amepewa zoezi la kujifunza kila siku usiku kufa na asubuhi kufufuka lakini wengine zoezi hilo lilipitiliza wakafa kweli lakini wewe u-mzima hadi leo. Tumepona magonjwa, ajali, matatizo mbalimbali, ni kwa neema yake BWANA. Hivyo, mwanadamu kumbuka kumwambia BWANA asante.

Sadaka ya shukrani ni muhimu sana hasa unapotoa kwa kumaanisha. Maana wako wengi wanatoa sadaka wala hailingani na tendo. Ukisoma Luka 17:11-19 utaona jinsi YESU alivyowaponya watu kumi wenye ukoma lakini mmoja tu kati ya wale kumi ndiye alionyesha moyo wa shukrani kwa YESU, alirudi akimtukuza MUNGU na kumshukuru.

Je, wewe mwenzangu unakumbuka kutoa sadaka ya shukrani kwa BWANA MUNGU?

BARIKIWA SANA.

Monday, 16 April 2012

SADAKA YA DHABIHU

Sadaka ya dhabihu ni sadaka kama nyingine isipokuwa sadaka hii ya dhabihu mara zote huwa inagusa kitu, mtu, vitu vya thamani ambavyo mwenye kuambiwa kutoa huwa anavipenda sana. Sadaka inayogharimu sana hata kuleta maswali.

Sadaka hii mara nyingi BWANA mwenyewe husema nawe kwamba "Nipe", tena BWANA hutaka kwa maana anajua unayo na unaweza kutoa. BWANA anaweza kutaka kwako utoe mfano gari, nyumba, fedha kwa ajili ya jambo fulani. Kitu ambacho moyo wako utauma katika kutoa.
Watu wengi wameshindwa kuwa watii kwanza kwa sababu walivyoambiwa kutoa walivipenda vile vitu au kile kitu. Hawakuamini kuwa ni sauti ya MUNGU japo sauti hiyo ilirudia mara kadhaa kwao.

Pia sadaka hii ya dhabihu MUNGU hukuelekeza mahali pa kutoa na kuipeleka. Inawezekana ikawa kwa ajili ya wajane, yatima, wasiojiweza, kanisani, au kwa mtumishi fulani wa MUNGU. Mpendwa, tii sauti ya BWANA na chukua hatua, pekela. Sadaka hii ina ulinzi na mafanikio.

Lakini pia mtu wa MUNGU anaweza kutumiwa na BWANA mwenyewe kukutaka wewe utoe sadaka hii ya dhabihu, tii na utoe ikiwa moyoni una amani na utapata kibali toka kwa BWANA.
Biblia inawataja watu wachache sana waliokuwa watii na wakatoa sadaka hii ya dhabihu walipoambiwa na MUNGU. Japo iliwauma lakini kwa kutii sauti ya MUNGU waliweza kutoa.

Kwanza kabisa, MUNGU mwenyewe kutoa sadaka hii ya dhabihu. MUNGU ilimuuma sana lakini aliitoa kwa ajili yetu sisi wanadamu. Yohana 3:16 Alimtoa YESU KRISTO kwa ajili yetu. Kwanza, ilikuwa ni kulipa deni la dhambi za wanadamu wote. Pili, kumpatanisha mwanadamu na MUNGU. Tatu, kumrudishia mwanadamu nafasi ya awali kwa MUNGU ambayo iliharibiwa na dhambi. Warumi 5:9-11. Waebrania 9:28, Waebrania 10:3-7.

Mtu wa pili kutoa sadaka ya dhabihu alikuwa rafiki wa MUNGU, Ibrahim. Mwanzo 22:1-18. Ibrahim aliambiwa kumtoa mwanawe Isaka, mwana wa pekee. Lakini kwa kuwa alijifunza kutii ,alikubali kumtoa. Tafakari sana yale maneno ya Mwanzo 22:15-18.

Mtu wa tatu ni mwanamke mjane wa Serepta. Huyu hakuambiwa na BWANA. Huyu anaambiwa na mtu wa MUNGU Eliya kutoa kwa ajili ya nafsi yake. Sadaka hii ya dhabihu inaweza kutolewa kwa ajili ya matumizi ya mtumishi au watumishi wa MUNGU. 1Wafalme 17:10-16.

Mjane huyu alitii sauti ya mtumishi wa MUNGU akafanyia chakula kwanza kwa ajili yake. Kwa kule kumlisha Eliya, MUNGU akafanya kwa ajili yake na  nyumba yake kwa siku nyingi. Ayubu 8:6.

Mtu wa nne ni mwanamke mjane. Huyu aliyemwona ni BWANA YESU mwenyewe wakati wa kutoa sadaka ya shukrani kuu. Lakini huyu anatoa dhabihu. Luka 21:1-4.
Kila anaetoa sadaka ya dhabihu kwa moyo wa utii huyo ana baraka na ulinzi wa MUNGU mwenyewe.

BARIKIWA.

Wednesday, 11 April 2012

SADAKA YENYE HAFURU INAFANYA UKUMBUSHO KWA MUNGU

Kwa habari ya utoaji wa sadaka na kupata kibali na baraka, haijalishi kama wewe umeokoka au hujaokoka ila umesimama katika ahadi za MUNGU za kumjaribu katika kutoa, hapo MUNGU ni lazima kubariki na upate kibali kwake.

Biblia inawataja watu wachache waliokuwa waaminifu katika kutoa sadaka wakiambatanisha na maombi yao kwa MUNGU. Kumbuka sadaka yenye kumgusa MUNGU iliyoambatanishwa na maombi, MUNGU anaiona na kuikumbuka na kutoa jibu kwa hilo hitaji lako.

Ukisoma Matendo 10:1-4, 31, utamuona mtu mmoja jina lake Kornelio. Huyu alikuwa askari wa kikosi kiitwacho Kiitalia. Pamoja na nafasi yake ya uaskari, Kornelio alikuwa na sifa za kumcha MUNGU yeye na watu wa nyumba yake. Pili, Kornelio alikuwa na sifa ya utoaji wa sadaka na kuwapa watu maana hakuwa Mkristo lakini alimjua na kumwomba MUNGU.

Kwa matendo ya Kornelio, watu wa nyumbani wake na majirani wakapata wokovu kwa kubatizwa kwa jina la YESU. Hapa tunaona sadaka na maombi ya Kornelio ziliwaokoa wengi. Pia hata wewe unaweza kuokoa watu wa nyumbani mwako, ukoo wako,kazini kwako, nk. kwa kutoa sadaka na kusemea.

Mtu wa pili ambaye kwa njia ya utoaji wa sadaka zake kwa uaminifu kuliweza kumrudishia uzima wa mwili huu ni Dorkasi. Matendo 9:36-39.

Huyu ananenwa kwa sifa ya kuwa na matendo mema na utoaji wa sadaka na kulihudumia Kanisa la MUNGU kwa kuleta vitambaa na nguo Madhabahuni kwa BWANA. Huyu alikufa wajane wakapeleka ujumbe kwa Petro kwamba aje. Naye kwa kuwa alikuwa muaminifu mbele za BWANA alirudishiwa uzima.

Mtu wa tatu ni Akida. Huyu naye alikuwa ni askari, mtu aliyejaa matendo mema kwa Taifa na utoaji wa sadaka kwa ajili ya kazi ya BWANA. Mtumwa wake aliumwa, na alikuwa nampenda sana mtumishi wake. Kwa imani yake kubwa aliyokuwa nayo, Mtumwa wake alipata kupona. Luka 7:2-10. Je ni wangapi wanawapenda watumishi wa nyumbani mwao?

YESU alikwenda kwa sababu alisikia sifa za huyu Akida kwamba amejenga nyumba ya kuabudu, anastahili kutendewa jambo hili analoliomba. Isaya 38:1-5.

Sadaka zetu tunazozitoa kwa moyo kabisa zina ushawishi mkubwa mbele za BWANA naye atafanya tu.

Kila sadaka unayotoa mbele za MUNGU inafanya ukumbusho. Kumbuka pia upo ukumbusho mbaya mbele za MUNGU kwa sadaka tuzitoazo. Tumwangalie kama ilivyokuwa kwa Kaini. Mwanzo 4:3-7. Pia tazama Malaki 2:2.

Daima toa sadaka inayomtukuza MUNGU wako. Zaburi 50:23

BARIKIWA

Monday, 9 April 2012

UHUSIANO WA SADAKA YAKO KWA MUNGU

Uko uhusiano mkubwa sana wa mtoaji sadaka na MUNGU wake. Sadaka yako inakujengea wewe mtoaji na MUNGU mpokeaji uhusiano mkubwa sana wa kibaraka, kukubarika na MUNGU ikiwa sadaka yako imegusa moyo wa MUNGU kweli.

Lakini pia uko uhusiano mkubwa sana kwa yule mtoaji wa sadaka kwa miungu au kwa waganga. Sadaka yako au fedha yako au wanyama wako unaoagizwa na huyo mganga kutoa hakika unajenga uhusiano nae.

Sadaka yako inajenga na kuimarisha agano kati yako na MUNGU. Anachokifanya MUNGU kwako ni kikubwa mno hasa ni kuachilia baraka za Ibrahimu zikujie na ulinzi wake. Na ikiwa sadaka zako unapeleka kwa miungu hakika ujue kuwa wewe ni mtumwa wa shetani na baraka uzipatazo ni za kitambo kifupi sana tena zimejaa masharti mengi.

KUMBUKA, mahali fedha yako au sadaka yako ilipo ndipo na moyo wako ulipo, palipo na moyo wako ndipo na imani yako ipo. Mathayo 6:21, Luka 12:34.

Ni kweli fedha yako ilipo hapo na moyo wako upo hapo, kama kwa MUNGU moyo wako uko kwake. Kama umewekeza kwa mganga daima moyo, imani yako ipo huko. Hiyo fedha imekujengea mahusiano na huyo mganga.

KANUNU SABA (7) ZA UHUSIANO WA SADAKA ZAKO KWA MUNGU

1. Kibiblia, sadaka zako unazotoa kwa MUNGU huwa zinakufanyia agano la mahusiano na MUNGU hasa pale unapotia sadaka yenye harufu nzuri ya kumridhisha MUNGU. Mwanzo 8:20-21. MUNGU akasema na kufunga agazo na Nuhu kwamba hatailaani nchi tena. Nuhu alitoa sadaka iliyogusa moyo wa MUNGU. Malaki 2:2-5.

2. Sadaka inakufanyia upatanisho na MUNGU. Sadaka inakufutia dhambi, sadaka inakujengea daraja wewe la kumfikia MUNGU, sadaka inakuhuhisha na MUNGU wako. Warumi 5:9-10, Yeremia 32:36-41.

3. Sadaka inaonyesha upendo wako ulivyo kwa MUNGU wako. Sadaka yako inaonyesha moyo wako ulivyo, uaminifu wako ulivyo kwa MUNGU wako. Hivyo, kwa njia ya sadaka zako unaweza kuona jinsi uhusiano wako ulivyo na MUNGU.

Tukumbuke sana habari ya Kaini na Habili. Mwanzo 4:3-7, Luka 21:1-9. Habili anapata kibali na Kaini anapata laana na alama. Tujiulize, sadaka zetu zinapata kibali au laana na alama? Malaki 2:2-5.

4. Sadaka yako inaonyesha moyo wako wa shukrani kwa MUNGU wako jinsi ulivyo. Kumbuka MUNGU amekutendea mambo mengi katika maisha yako kutoka kuzaliwa, kukua, kazini kwako. Sadaka pekee ndio inakuonyesha moyo wako wa shukrani kwake na ndipo MUNGU anatengeneza uhusiano wake na wewe. Zaburi 116:12, Zaburi 136:1, Mithali 8:18.

5. Sadaka yako unayotoa inakuonyesha wewe jinsi unavyomheshimu MUNGU wako kwa vyote ambavyo MUNGU amekufanyia maishani mwako. Kwa mafanikio yako yote unapaswa kumheshimu MUNGU. Mithali 3:9, 3Yohana 1:2, Zaburi 116:12.

6. Sadaka yako inaonyesha utii wako kwake kwa kile ulichokisikia. Kutoa kwako kunaonyesha utiifu wako kwake, hivyo MUNGU kupitia sadaka yako anaimarisha uhusiano wako naye. Kumb. 28:1, Yohana 17:21-24.

7. Sadaka yako inakutambulisha kuwa vyote ulivyonavyo ni mali ya MUNGU, tumepewa kama mawakili tu. Hivyo kutoa kunaonyesha uaminifu wetu kwa MUNGU. Zaburi 24:1, 1Korintho 4:1-2.

BARIKIWA

Saturday, 7 April 2012

KUTOA SADAKA

SADAKA NI NINI?

Sadaka ni aina ya matoleo yanayotolewa na mwanadamu kwa maana ya kumrudishia MUNGU wake shukrani. Tena ni agizo la MUNGU mwenyewekwa mwanadamu kuwa atoe kwa kupenda. Kutoka 25:1-3

AINA ZA SADAKA

Ziko aina nyingi za sadaka ambazo MUNGU ameagiza kutoa kwake nazo ni:-

1. Sadaka ya kawaida. Hii inaitwa shukrani ambayo mwanadamu anatoa kumshukuru MUNGU kwa ulinzi, amani, upendo, kuongozwa na kutunzwa naye kwa mambo mbalimbali kwa wiki nzima, ambapo huja Jumapili kutoa sadaka.

2. Zaka au fungu la kumi. Hii ni lazima kutoa tena kamilifu. Hii hutolewa kanisani kwa Kuhani. Malaki 3:10

3. Nadhiri au ahadi. Soma Kumb. 23:21-23

4. Shukrani kwa yale uliyotendewa naye. Mfano, kupona katika ugonjwa, kupata kazi, kufunga ndoa, nk. Zaburi 136:1.

5. Dhabihu. Hii mara nyingi MUNGU husema nawe moja kwa moja. Mwanzo 22:1-3

6. Malimbuko. Kila kitu cha kwanza, mfano, mshahara wako wa kwanza wote ni sadaka kwa MUNGU, toka shambani mazao ua mifugo, biashara ile faida ya mapato ya kwanza ni mali ya MUNGU. Nehemia 12:44, Kumb. 26:1-2, 10-11, 2Nyakati 31:4 - 6.

7.Mavuno. sadaka hii hutolewa mara moja toka katika mshahara wako, shambani, biahsara zako. Kumb. 26:1-2, 10-11

8. Sadaka ya dhambi

9. Sadaka ya upatanisho.

Sadaka hizi mbili na. 8 na na. 9, kwa sasa hazipo kwa sababu BWANA YESU ametulipia deni la dhambi na ametuatanisha na MUNGU kwa njia ya mauti yake pale msalabani. Soma Warumi 5:9-10, Walawi 17:11.

Kwa kufuata Biblia, hizi ndizo tunaziita sadaka ambazo kila Mkristo anapaswa kuzijua na kutoa kwa wakati.

TUNATOA WAPI SADAKA?

Sadaka kama sadaka tunatoa nyumbani mwa BWANA maana ndipo mahali sahihi pa kupeleka sadaka yako kwa maana hapo ndipo tunakutana na BWANA. Kumb. 12:5-7.

Wakati wa kupeleka na kutoa sadaka yako hakikisha kwamba sadaka yako inaambatana na maombi ya uhitaji wako au shukrani zako.

KWANINI TUNATOA SADAKA?

1. Tunatoa sadaka kama agizo la MUNGU mwenyewe. Kumb. 8:6, Kutoka 25:1-2

2. Tunatoa sadaka kuonyesha utii kwa MUNGU wetu wa upendo. Kumb.28:1, Isaya 43:4

FAIDA YA KUTOA SADAKA

Ziko faida nyingi azipatazo mwanadamu kwa kutii na kuwa mwaminifu katika kutoa;- baraka, ulinzi, afya, nk. Malaki 3:10, Kumb. 28:1-4, 2Nyakati 31:10b, Kumb. 28:7-10

HASARA ZA KUTOKUTOA SADAKA

MUNGU anaruhusu kila aina ya ubaya ya madhara yanayokupata wewe, mf. magonjwa. MUNGU anaondoa ulinzi kwako na katika maeneo mbalimbali yanayokuhusu, mf. kazini, kwa watoto, mali zako, nk. Kumb. 28:20, 45-48

BWANA atusaidie katika kukumbushana na atusaidie kutenda mema, kuwa watii na kuwa watendaji wa Neno.

BARIKIWA